Loading...
Rais Magufuli Akerwa na Uozo Uliopo Ndani ya CCM Mwanza.......Aagiza Jiji la Mwanza Lisiwatoze Kodi Wafanyabiashara Wadogowadogo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuna mambo ya hovyo ambayo yapo ndani ya Chama cha Mapinduzi ambayo yanahitaji kuhojiwa na kupatiwa majibu yenye tija.
Aikihutubia maelfu ya wananchi jana waliojitokeza kumsikiliza katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza Dkt. Magufuli alisema anafahamu kwamba ndani ya CCM kuna mambo ya hovyo na mfano ni uwanja wa CCM Kirumba na majengo mengine ya CCM ambayo ukiuliza maduka na ofisi zinazozunguka majengo hayo mapato yake yako wapi huwezi kupata majibu ya kuridhisha.
"Ninyi wananchi wa Mwanza na wanachama wa CCM hojini haya na atakayewauliza mwambieni ni mimi Mwenyekiti wa CCM nimesema muwaulize, nataka chama ambacho mali zake zinajulikana kwa sababu ukienda kuwauliza mnakusanya shilingi ngapi kwa chumba kimoja wanaweza kukuambia ni elfu 50 kumbe wanaingiza laki 5" Alisema Rais Dkt. Magufuli
Rais Magufuli alisisitiza kwamba anaitaka CCM ya Rais wa kwanza wa Tanzania Mwl. Julius Nyerere siyo CCM ya watu ambao mchana wapo CCM na usiku wapo vyama vingine, wanaofanya hivyo ni bora wahamie huko moja kwa moja.
Aidha katika hatua nyingine Rais Dkt. Magufuli ameagiza uongozi wa Jiji la Mwanza kutowatoza ushuru wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwa wanatakiwa wanufaike na taifa lao na pia wamachinga waachwe mjini kwanza hadi hapo watakapo andaliwa mazingira mazuri ya kufanyia biashara yatakayokuwa na wateja.
Filed Under:
habari
Shibuda .....Awapa Neno UKAWA
Katibu Mkuu wa Chama cha ADA-Tadea, John Shibuda jana alijitokeza katika mkutano wa Rais Dkt. John Magufuli katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza na kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa namna ambavyo anatatua kero za wananchi.
Akihutubia maelfu ya wakazi wa Mwanza na maeneo jirani waliojitokeza kumsikiliza Rais Dkt. Magufuli , Shibuda alivitaka vyama vingine vya siasa nchini kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kuwa kazi anayoifanya ni kwa ajili ya watanzania wote.
"Mheshimiwa Rais Magufuli endelea kuwahudumia watanzania na nikuambie sijawahi kuona mchongoma unang’olewa kwa upepo au sijawahi kuona utelezi wa mlenda unamwangusha mtu mzima" - Alisema Shibuda.
Shibuda alisema vyama vya UKAWA vinapaswa kutambua kwamba Rais Dkt. Magufuli ni mtu mzuri ndiyo maana aliwasaidia kumaliza mgogoro wa uchaguzi wa Meya Jijini Dar es Salaam hivyo watambue mchango wake kwa taifa .
Aidha Shibuda alimuomba Rais Magufuli kwamba akipata muda aende akamweleze vizuri matatizo yanayowakabili wakulima nchini.
Filed Under:
habari
PICHA: Rais Magufuli Akiweka Jiwe La Msingi Daraja Wa Waenda Kwa Miguu La Furahisha Pamoja Na Upanuzi Wa Barabara Ya Mwanza Airport
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha kuwa ujenzi wa daraja la watembea kwa miguu na upanuzi wa Barabara ya Makongoro jijini Mwanza unakamilika ifikapo disemba mwaka huu.
Aidha amesema upanuzi wa barabara ya Makongoro uliokuwa ujengwe kati ya Furahisha hadi Pasiansi Km 2.8 sasa utaendelezwa hadi kufikia uwanja wa ndege.
Akizungumza jana mara baada ya kuweka jiwe la msingi la daraja la watembea kwa miguu na upanuzi wa barabara ya Makongoro Mh. Dkt. Magufuli alisema kasi ya ujenzi wa barabara jijini Mwanza uendane na ujenzi wa uwanja wa ndege ili kuwezesha mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha nchi za maziwa makuu.
“Nakuagiza Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano uhakikishe kuwa barabara na daraja la watembea kwa miguu Furahisha vinakamilika mwezi desemba na mkandarasi wa uwanja wa ndege anaanza kazi mara moja”. Alisisitiza Rais Dkt. Magufuli.
Alisema nia ya Serikali yake ni kununua meli mbili na kujenga daraja kati ya Kigongo na Busisi ili kuboresha huduma za usafiri katika Ziwa Victoria.
Naye Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale alimtaka mkandarasi anaejenga daraja la waenda kwa miguu na barabara ya Makongoro kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Zaidi ya shilingi bilioni 6.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo utakaopunguza msongamano wa magari na ajali katika barabara ya makongoro jijini Mwanza.
Aidha amesema upanuzi wa barabara ya Makongoro uliokuwa ujengwe kati ya Furahisha hadi Pasiansi Km 2.8 sasa utaendelezwa hadi kufikia uwanja wa ndege.
Akizungumza jana mara baada ya kuweka jiwe la msingi la daraja la watembea kwa miguu na upanuzi wa barabara ya Makongoro Mh. Dkt. Magufuli alisema kasi ya ujenzi wa barabara jijini Mwanza uendane na ujenzi wa uwanja wa ndege ili kuwezesha mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha nchi za maziwa makuu.
“Nakuagiza Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano uhakikishe kuwa barabara na daraja la watembea kwa miguu Furahisha vinakamilika mwezi desemba na mkandarasi wa uwanja wa ndege anaanza kazi mara moja”. Alisisitiza Rais Dkt. Magufuli.
Alisema nia ya Serikali yake ni kununua meli mbili na kujenga daraja kati ya Kigongo na Busisi ili kuboresha huduma za usafiri katika Ziwa Victoria.
Naye Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Patrick Mfugale alimtaka mkandarasi anaejenga daraja la waenda kwa miguu na barabara ya Makongoro kuhakikisha ujenzi wake unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Zaidi ya shilingi bilioni 6.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo utakaopunguza msongamano wa magari na ajali katika barabara ya makongoro jijini Mwanza.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, Mbunge wa Sumve Richard Ndassa wakipiga makofi mara baada ya tukio la uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Daraja la waenda kwa miguu la Furahisha pamoja na Upanuzi wa barabara ya Mwanza-airport.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale akitoa maelezo ya namna daraja la Furahisha litakavyokuwa mara baada ya kukamilika.
Filed Under:
habari
Mbowe Achiwa Kwa Dhamana.......Tundu Lissu Asisitiza Oparesheni UKUTA Iko Palepale
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema licha ya viongozi wa chama hicho kutishwa, kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, bado msimamo wao kuhusu operesheni Ukuta itakayofanyika Septemba Mosi mwaka huu uko pale pale.
Chama hicho kinatarajiwa kufanya operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).
Operesheni hiyo inatarajiwa kuwa itakwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya hadhara nchi nzima, ambayo itafanyika Septemba Mosi, mwaka huu.
Hatua hiyo imefikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa siku nne mfululizo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio matatu ambayo yatatekelezwa na chama hicho.
Pamoja na mambo mengine, chama hicho kimesema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na kuachiwa kwa dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwanasheria Lissu alisema msimamo wao uko palepale na hakuna kilichobadilika.
“Wamemuhoji kwa taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama wa kufanya mkutano nchi nzima. Tatizo jeshi letu wakisikia maandamano, mkutano au mtu anamsema Magufuli basi anatuhumiwa kwa uchochezi, wametumia muda mrefu kumuhoji lakini mwisho wamemwachia kwa dhamana na amewahi ‘Airport’ ili aende kuhudhuria mazishi ya kamanda wetu Senga (Joseph) na watamwita watakapomwihitaji tena,” alisema Lissu.
Alisema pamoja na hayo bado msimamo wa chama hicho kufanya mikutano waliyoiita Operesheni Ukuta ipo pale pale ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.
“Nafikiri ni muhimu sana huko tunapoenda kuzungumza na wenzetu hii kitu inaitwa uchochezi ni nini? Tunashitakiwa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo waliingiza vifungu vya uchochezi mwaka 1978 lengo lao kuu ni kuwafunga watu midomo na ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja.
“Hata hivyo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ndiye wa kwanza kushtakiwa kwa uchochezi pamoja na mwandishi Robert Makenge na mwenzao Rashid Bagedae, kwa msingi huo sisi tunafuata nyayo zake,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema kuitwa mchochezi, ni jambo la ufahari kupinga udikteta kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.
“Nasema hivyo kwa sababu Mwalimu Nyerere ndiye wa kwanza kuitwa mchochezi, ni kitendo cha kufunga watu midomo ili washindwe kuwaita watu wajinga pale wanapofanya ujinga.
“Tume ya Jaji Nyalali mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi unatambulishwa na kuanza nchini ilipendekezwa sheria hii ifutwe kwa sababu haiendani na mfumo uliopo lakini hakuna kilichofanyika,”alisema.
Mwanasheria huyo ambaye naye amefunguliwa kesi ya uchochezi katika Mahakama ya Kisutu jijini Dar, aliwataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi Agosti 2, mwaka huu mahakamani hapo.
“Dawa yao si majaji bali umma… umma ufurike, tutawashinda hawa watu makesi yenyewe ni haya ambayo hayana kichwa wala miguu,”alisema na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Mbowe alifika kituoni hapo akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa Chadema akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambaye hata hivyo alizuiwa kuingia katika chumba cha mahojiano.
Askari waliokuwa kwa wingi katika eneo hilo, walisikika wakisema kuwa anayepaswa kuingia ndani ni Mbowe, Mwanasheria Tundu Lissu na Wakili wa Chadema, John Mallya.
Lowassa, wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari walilazimika kubaki nje huku askari wakiimarisha ulinzi wakiwa wamebeba bunduki zao huku magari yenye maji ya kuwasha yakiwa yameegeshwa pembeni.
Wakati chama hicho kikijiandaa kutekeleza Operesheni Ukuta Septemba Mosi, tayari Rais Magufuli amezuia operesheni hiyo na kuwaonya wale wote watakaokaidi agizo lake na kuamua kuandamana.
Filed Under:
habari
Mkurugenzi wa Bagamoyo Aliyetumbuliwa na Rais Magufuli ameponzwa na Kesi za Uchaguzi zilizoipa ushindi Chadema
Mkurugenzi wa Sheria wa Chadema, Peter Kibatala amempa pole aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Azimina Mbilinyi kwa kuenguliwa kwenye nafasi hiyo, ikiwa ni siku moja baada ya kesi za uchaguzi alizotolea ushahidi wilayani Kilombero kuhukumiwa.
Akiandika katika ukurasa wake wa Facebook jana, Kibatala alisema:“Tunasikitika nawe, na kukupa pole nyingi sana.”
Katika ujumbe huo aliothibitisha baadaye kuuandika, Kibatala aliongeza:“Tunakushukuru sana kwa kutoa ushahidi wa ukweli na wa haki katika kesi za uchaguzi majimbo ya Kilombero na Mlimba yaliyotolewa hukumu jana (Julai 29).”
Wakili hiyo aliongeza: “Wakati wa Uchaguzi Mkuu ulikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero na Msimamizi wa Uchaguzi katika Majimbo waliyoshinda Chadema.”
Juzi, taarifa ya Ofisi ya Rais–Tamisemi iliyotolewa na Katibu Mkuu, Mussa Iyombe bila kufafanua sababu za kuenguliwa kwake, ilieleza kwamba Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mbilinyi kwa sababu hakuridhishwa na utendaji wake wa kazi.
Mbilinyi alikuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilombero kabla ya kuhamishiwa Dodoma na baadaye Bagamoyo.
Alipotafutwa kuthibitisha maneno yaliyoandikwa kwenye ukurasa wake wa facebook, Kibatala alisema: “Ni kweli niliandika kwenye ukurasa wangu wa facebook na ninaomba maneno hayo yabaki kama yalivyo, naona watu wengine wameanza kutafsiri vinginevyo.”
Katika hukumu hizo, Majaji Projest Rugazia na Penterine Kente waliwapa ushindi wabunge wawili wa Chadema, Susan Kiwanga na Peter Liajualikali baada ya kukosekana ushahidi wa kutengua matokeo hayo.
Juhudi za kumtafuta Mbilinyi kuzungumzia hatua iliyochukuliwa dhidi yake hazikuzaa matunda kutokana na simu zake zilizopigwa mara nyingi kutokuwa hewani.
Filed Under:
habari
James Lembeli Aibukia Mkutano wa Rais Magufuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia wa wakazi wa Kahama mara baada ya kuwasili akitokea Nzega mkoa Tabora.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akicheza jukwaani wimbo wa kwaya ya Haleluya Kuu kutoka Kanisa la KKKT- Usharika wa Yeru Ndala Shinyanga kabla ya Kuhutubia mamia ya wakazi Kahama mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mbunge wa zamani wa Kahama James Lembeli mara baada ya kuwasalimia wananchi waliofika kwa ajili ya kumsikiliza Rais katika viwanja hivyo vya Kahama.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia wa wakazi wa Isaka mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ameambatana na Mbunge wa zamani wa Kahama James Lembeli ambaye ni mwanachama wa Chadema mara baada ya kumaliza kuhutubia mkutano mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akicheza pamoja na Wanakwaya wa Haleluya Kuu kutoka Kanisa la KKKT- Usharika wa Yeru Ndala Shinyanga mara baada ya kumaliza kuhutubia mkutano Kahama mjini mkoani Shinyanga.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia mara baada ya kuoneshwa picha na kijana mmoja aliyeishika picha hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia mamia ya wakazi wa Tinde mkoani Sinyanga. PICHA NA IKULU
Filed Under:
habari
Rais Magufuli....Sitogawa Chakula cha Bure Kwa Watakaopatwa na Janga la Njaa Bila Sababu za Msingi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema serikali yake haitagawa chakula cha bure kwa wananchi wanaopatwa na tatizo la njaa pasipo kuwa na sababu za msingi na badala yake amewataka watanzania wajikite kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kuzalisha chakula cha kutosha.
Rais Magufuli amesema hayo jana tarehe 31 Julai, 2016 wakati akihutubia mikutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake akiwa njiani kutoka Mkoani Tabora kuelekea Shinyanga na baadaye Geita anakoendelea na ziara yake.
Pamoja na kuwahimiza wananchi kuzalisha chakula cha kutosha ili kuondokana na njaa Rais Magufuli alisema serikali yake itajikita kuhakikisha inashughulikia tatizo la uhaba wa maji, ujenzi wa miundombinu hususani barabara na reli, kuimarisha huduma za matibabu, elimu na kutengeneza ajira.
Akiwa Isaka Mkoani Shinyanga Rais Magufuli alisema serikali haitalipa fidia kwa wananchi waliopatwa na maafa ya mafuriko yaliyobomoa nyumba zao mwezi Machi mwaka 2015 na badala yake itajielekeza kutatua tatizo kubwa la uhaba wa maji katika mji huo ambao una makutano ya reli ya kati ya kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda.
Katika Mji wa Kagongwa Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi dhidi ya vitendo vya ujambazi na ametoa siku tano kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha watu wanaojihusisha na ujambazi wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mjini Kahama, Dkt. Magufuli aliiagiza Wizara ya Nishati na Madini kushirikiana na Mbunge wa Kahama Mhe. Jumanne Kishimba kukokotoa mahesabu vizuri na kubaini kodi ambayo Serikali inastahili kulipwa baada ya Mbunge huyo kudai kuna kiasi kikubwa cha kodi hakijakusanywa kama ambavyo sheria inaelekeza.
Aidha, Rais Magufuli alisema serikali itahakikisha wawekezaji wanaochimba madini wanaacha kusafirisha mchanga wenye madini kwa lengo la kwenda kuchakata nje ya nchi na badala yake ametaka uchakataji huo ufanyike hapa hapa nchini.
Dkt. Magufuli alizungumza na wananchi vijiji vya Segese na Bukoli na kuwahakikishia kuwa Barabara ya Kahama, Segese, Kakola hadi Geita yenye urefu wa kilometa 146 itajengwa kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi.
Mjini Geita, Rais Magufuli alipokea kilio cha wananchi wanaodai kuwekewa zuio la kutumia mawe yenye mabaki ya madini ya dhahabu (Magwangala) kwa lengo la kusaga na kuchenjua ili kupata dhahabu, na ametoa wiki tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya tathimini na kuwaruhusu wachimbaji wadogo kutumia Magwangala.
Rais Magufuli pia ameiagiza Bodi ya Pamba hapa nchini kuhamisha ofisi zake zilizopo Jijini Dar es salaam na kuzileta katika Mikoa ya kanda ya ziwa ambako uzalishaji wa zao la pamba unafanyika.
Dkt. Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa bodi hiyo dhidi ya vitendo vya usambazaji wa mbegu za pamba zisizoota na amesema ikitokea tena watachukuliwa hatua.
Tarehe 01 Agosti, 2016 Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli anatarajia kukamilisha ziara yake ya siku nne katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Geita
31 Julai, 2016
Filed Under:
habari